Taasisi ya kusaidia sekta binafsi katika kilimo (PASS) ambayo inashirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuendesha Kituo cha Ubunifu wa Kilimobiashara kwa Vijana (SUA - AIC) ambacho ni Idara ndani ya Taasisi ya PASS Trust, kilichopo SUA mkoani Morogoro, imekishukuru Chuo hicho cha SUA, Serikali ya Kifalme ya Denmark, na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwaatamia na kuwapatia ujuzi vijana ili kukabiliana na upungufu wa ajira nchini kupitia Sekta ya Kilimo.
Shukrani hizo zimetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa PASS Trust Prof. Sylvia Temu, wakati akizungumza katika ziara akiwa na Wajumbe wengine pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo walipokitembelea kituo hicho kilichopo katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine - Morogoro.
Prof. Temu amesema kuwa, PASS Trust wamefurahishwa na juhudi za vijana hao takribani 40 kwa kujituma na kuwekeza muda wao kwa mwaka mmoja na nusu katika shughuli za kilimo kwenye kituo hicho, na hiyo inaonyesha wana maono na malengo.
"Lengo letu kubwa la kuja kutembelea kituo hiki ni kuja kujionea kwa macho kinavyoendelea, kujifunza, na kuona ni changamoto gani zilizopo ili kwa pamoja kwa kushirikiana na SUA tuweze kuona namna ya kuzitatua" amesisitiza Profesa Temu.
Ameongeza kuwa wameyaona baadhi ya mazao yanayolimwa na vijana hao ambayo ni pilipili hoho za rangi, matango, na matikiti matamu; Na changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni ukosefu wa maji ya kutosha kutokana na athari za ukame.