WABUNGE WATEMBELEA KITUO CHA UBUNIFU WA KILIMOBIASHARA KWA VIJANA (SUA - AIC)

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imetembelea Kituo cha Ubunifu wa Kilimobiashara kwa Vijana (SUA - AIC) ambacho ni Idara ndani ya Taasisi ya PASS Trust, kilichopo SUA mkoani Morogoro. Kituo hiki kina malengo yafuatayo kwa vijana: Kumfanya kijana aweze kuanzisha, kuendesha na kumiliki biashara binafsi kwa lengo la kutengeneza faida, Kumpatia kijana ujuzi, ufahamu, uzoefu, na ushauri juu ya njia bora na za kisasa za ujasiriamali, uendeshaji wa kilimobiashara, utafutaji wa masoko na masuala ya kiufundi kwenye kilimo cha mbogamboga, pamoja na, Kumuunganisha kijana mjasiriamali na taasisi za kifedha ikiwemo benki ili kuweza kupata mkopo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza biashara yake akiwa anajitegemea baada ya kutoka kwenye kituo atamizi.


Mkurugenzi wa Fedha na Utawala - PASS Trust, Doreen Mangesho akielezea kuhusu Kituo cha Ubunifu wa Kilimobiashara kwa Vijana (SUA - AIC).

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala PASS Trust, Doreen Mangesho ameelezea namna Taasisi ya PASS Trust inavyoshirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika usimamizi na uendeshaji wa Kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2018, mpaka sasa vijana 285 (wanawake 144 na wanaume 141) wameshahatamiwa. Ambapo, baada ya kuhitimu PASS Trust huwawezesha kupata huduma ya dhamana ya mikopo ya kilimobiashara kupitia benki washirika. Baadhi ya vijana wamepata fursa ya kujiunga na programu ya vijana ya Building a Better Tomorrow (BBT) inayoenda kuwapa fursa ya kuongeza ujuzi na kumiliki ardhi kwa ajili ya kufanya kilimo, suala ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa vijana wengi.


Kijana Mjasiriamali, Amos Ndarahwa Masune akielezea namna anavyofanya kilimobiashara cha pilipili za rangi kwenye shamba nyumba katika Kituo Atamizi.

Kamati hii yenye wajumbe 21 chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Prof. Kitila Mkumbo imefanikiwa kujionea namna vijana wanavyofanya shughuli za uzalishaji kuanzia shambani hadi sokoni. Vilevile, vijana wajasiriamali wameelezea namna wanavyofanya shughuli zao za kilimobiashara cha mbogamboga na matunda.