Yohane Kaduma Amehudhuria Hafla ya Uwekaji Jiwe la Msingi Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta Tanzania

Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Yohane Kaduma, amehudhuria tukio kubwa la uwekaji jiwe la msingi kiwanda cha kuunganisha matrekta Tanzania. Kiwanda hiki cha uunganishaji matrekta kinajengwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Kitanzania ya Agricom Africa Ltd na Mahindra Mahindra ya nchini India ambayo ni kampuni kubwa duniani kwa uzalishaji wa Matrekta.

Jiwe la msingi limewekwa na Mgeni rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Maadhimisho na Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane 2024 yaliyofanyika jijini Dodoma kitaifa. Uwekezaji huu ni matokeo ya ziara ya Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India mwezi Oktoba 2023, ambapo, aliialika Kampuni ya Mahindra kuanzisha kiwanda cha uunganishaji matrekta nchini Tanzania.

Kiwanda hiki kitakuwa ni kiwanda cha kwanza cha uunganishaji wa matrekta katika ukanda wa Afrika Mashariki. Kiwanda kipya kinatarajiwa kukamilika mwaka 2025, na kinatarajiwa kuzalisha matrekta 10,000 katika miaka 5 ijayo. Pia kiwanda hiki kipya kitahudumia nchi jirani za Afrika, kikiimarisha kujitegemea katika uunganishaji na usambazaji wa matrekta katika ukanda huu.

PASS Trust ni mdau mkubwa katika uwezeshaji wananchi kiuchumi hasa katika utoaji wa dhamana za mikopo ya kilimo biashara; Ambapo, PASS Trust imekuwa ikishirikiana na Kampuni ya Agricom Africa Ltd katika kuwawezesha wajasiriamali wa kilimo biashara kumiliki zana za kilimo kwa kuwaongezea dhamana. Dhamana hizo ndizo zinazowawezesha kupata zana kama matrekta, powertillers n.k kutoka Kampuni ya Agricom Africa.